Chombezo : Baba P...Baba Pili...Baba Pilima!
Sehemu Ya Tano (5)
Kulipokucha kabisa, ndiyo kwa mbali akapitiwa na usingizi. Mama Pilima wakati anaamka alishangaa kumwona mumewe bado kitandani wakati anavyojua, huwa anatangulia kuamka siku zote. Alimwamsha…
SHUKA NAYO MWENYEWE SASA…
“Baba Pilima…baba Pilima.”
Baba Pilima alishtuka na kumtumbulia macho mke wake…
“Mbona leo mpaka muda huu bado umelala, una nini mume wangu?”
“We mama Pilima aisee ni kiboko,” alisema baba Pilima huku akiendelea kumwangalia mkewe…
“Kwa nini mume wangu?”
“We tambua hivyo tu.”
Maneno ya baba Pilima yalimsumbua sana mke wake kiasi kwamba, muda huohuo aliwaza mambo yasiyopungua mia kidogo…
“Mh! Au amejua kitu? Lakini kama amejua kitu amejuaje? Mbona ni mambo ya siri sana?”
Alikuwa na shida ya shilingi elfu hamsini asubuhi hiyo lakini akashindwa kumwambia mume wake.
Dakika zilipita, mambo mengine yakaendelea huku baba Pilima akiamua kuingi mzigoni yeye mwenyewe.
Akiwa mjini, baba Pilima alishika simu yake akasachi namba ya baba Pili, akamwendea hewani…
“Haloo,” alipokea baba Pili…
“Mkubwa salama?” alisalimia baba Pilima…
“Salama bwana…nani?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mimi naitwa Emmanuel, nimepewa namba yako na jamaa anaitwa Sudi, kuna biashara fulani alisema unaweza kunielekeza.”
“Sudi? Sudi…Sudi…Sudi…Sudi yule wa Kigamboni?”
“Sijajua anaishi Kigamboni au la!” alijibu baba Pilima…
“Wewe uko wapi?” aliuliza baba Pili…
“Kariakoo…”
“Na mimi nipo Kariakoo. Nipo hapa DDC, njoo basi tuonane ana kwa ana,” alisema baba Pili…
“Oke.”
Lakini wakati baba Pili akimsubiri baba Pilima aliamua kumpigia simu Sudi aliyemjua yeye ili amuulize vizuri kuhusu baba Pilima, lakini jamaa simu yake haikuwa hewani.
Mara, baba Pilima aliingia kwenye Ukumbi wa DDC Kariakoo na kumpigia baba Pili. Naye baba Pili alipoona simu hiyo, akaangalia geti kubwa na kumwona baba Pilima simu ikiwa sikioni huku akishangaashangaa, akamwonesha ishara ya mkono kwamba, yeye yuko pale.
Baba Pilima alitembea hadi pale, akavuta kiti ili kukaa huku akimpa mkono baba Pili na kusema…
“Naitwa Emmanuel.”
“Oke, karibu sana. mimi naitwa Mutu.”
“Oke sawa.”
Kabla baba Pilima hajaanza kusema ya uongo, simu ya mama Pilima ikaingia kwa baba Pili…
“Sore bwana Emmanuel, ngoja nipokee simu ya nyumba ndogo yangu…”
“Sawa…sawa…”
“Haloo mama Pilima…eee! una shida na shing’ ngapi? Oke…mimi nipo DDC Kariakoo, njoo basi nikupe,” alitiririka baba Pili…
“Oke…oke,” akakata simu baba Pili…
“Unajua bwana Emmanuel kuwa na nyumba ndogo ni gharama sana! Yaani huwezi kumwambia huna pesa. Si unataka kulinda uhusiano!” alisema baba Pili huku akimwangalia baba Pilima…
“Enhe, umesema umepewa namba yangu na Sudi?” aliuliza baba Pili akikaa sawasawa pale kwenye kiti huku akijiona ni mwenye bahati ya madili ya mjini.
Kabla baba Pilima hajajibu, naye simu yake iliita…
“Sore, ngoja nipokee simu ya shemeji yako…halooo…eee! Nipo Kurasini….kuna nini..? haya…sawa,” akakata…
“Unajua bwana Mutu kuwa na mke ni lazima utumie akili sana! Na ni lazima umdanganye kidogo. Haitakiwi akajua sehemu rasmi uliyopo…si mmeshajuana tabia,” alisema baba Pilima huku akimwangalia baba Pili…
“Enhe, ulitaka kujua kama namba yako nilipewa na Sudi wa Kigamboni siyo?”
“Eee!”
“Mimi sijui kama anaishi Kigamboni, ila nilikutana naye Sinza,” alisema baba Pilima na kukohoa kidogo.
Lakini sauti yake ilionekana kuwa nzito tofauti na alivyofika, huenda ni baada ya kuuona usaliti wa waziwazi wa mkewe mama Pilima…
“Oke. Lakini chamsingi nadhani si anakoishi Sudi, ni hilo unalotaka nikusaidie maana mimi nina dili na mambo mengi sana, nadili na madini, nadili na ngozi, nadili na mbao, ila tu sidili na madawa ya kulevya,” alisema baba Pili na kuangalia lango kuu.
Kwa baba Pilima hiyo ilikuwa kama kumsukuma mlevi maana alijiuliza sana aingie na gia gani kwa mwanaume huyo ili amuelewe…
“Mimi nina biashara ya madini, madini orijino kabisa. Sasa Sudi akanipa namba na kusema nikikupigia tukikutana unaweza kunisaidia.”
“Unayo hapo?”
“No! Yapo nyumbani, ila nilitaka tukutane kwanza, maana naweza kuyafuata muda wowote ule,” alisema baba Pilima. Kabla baba Pili hajasema kingine chochote, simu yake iliita…
“Sore bwana Emmanuel, nina mgeni nadhani kafika, acha nimwambie aingie huku ndani…”
“Sawasawa, aingie tu,” alikubali baba Pilima…
“Ee mama Pilima mpenzi wangu…geti kubwa..? Oke…sasa ingia ndani basi, ukiingia tu utaniona nimekaa na jamaa yangu mmoja ni mfanyabiahara,” alifunguka baba Pili.
Baba Pili akakata simu haraka, kisha akawa anaangalia geti kuu wanaloingilia wateja akiamini mama Pilima ataingia muda huohuo ili ampe ishara kuwa, yeye amekaa palepale.
Mara, uso wa baba Pili ambaye alipokaa alikuwa akiangalia geti kuu, ulionekana kujaa tabasamu laini kuashiria kwamba, mgeni aliyemtarajia, sasa alikuwa anaingia ndani ya ukumbi huo wenye kukusanya watu wengine jijini Dar.
Mama Pilima alitangulia kumwona baba Pili kwani alipokaa uso wake ulikuwa dhahiri, lakini hakumwona mumewe aliyekaa kwa vile mgongo ndiyo uliangalia getini.
Mpaka anafika pale, alikuwa hajamtambua mumewe, hasa kutokana na mkao wake wa kuinamia meza. Inaonekana baba Pilima aliamua kukaa hivyo ili asigundulike haraka.
Mama Pilima, akiwa na uso uliojaa tabasamu la kujua anavuta mkwanja aliouomba, alianza kupeleka mkono kwa baba Pilima kwanza huku akisalimia kwa sauti yenye bashasha, tamu, ya kumtoa nyoka kwenye shimo lake…
“Mambo baby wa miye?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Poapoa, karibu sana mpenzi wangu…”
“Oke asante sweet,” alisema kisha akaachana na mkono wa mwenyeji wake huyo na kupeleka mkono kwenye mkono wa mumewe…
“Mambo anko?”
Mumewe aligeuka kiufasaha na kumwangalia mama Pilima usoni ili amwone sawasawa…
“Haaa!” alishtuka mama Pilima.
Mwili wote ulimwisha nguvu, akahisi kizunguzungu, akaanguka chini…puu! Mkoba kule, viatu huko!
“Bwana Emmanuel vipi tena? Mbona huyu mgeni wangu alipokuona wewe tu amepatwa na mshtuko?” aliuliza baba Pili huku akimtumbulia macho baba Pilima…
“Hata mimi sijui, aulizwe yeye, labda amenifananisha.”
Wateja wa baa hiyo walianza kujaa wakimzunguka mwanamke huyo, wengine wakisema ameshafariki dunia, wengine amezimia tu. Wapo waliobashiri kuwa, lazima mgeni wa baba Pili atakuwa anajuana naye tu.
Baba Pilima alitulia kimya akijifanya kweli hajui lolote lakini akimwangalia mkewe kwa macho yaliyojaa mshangao na kujikaza jambo f’lani la ndani sana!
Huduma ya kwanza ilitembea, watu wakatakiwa kukaa pembeni ili mwanamke huyo apate upepo kwa maana ye hewa safi ya oksijeni.
Baada ya dakika kumi na tano hivi, mama Pilima alishtuka. Kijasho chembamba kikimtoka. Alianza kwa kufumbua macho kwa kupepesapepesa huku akiendelea kulala kisha baadaye, akakaa.
Baada ya muda, baba Pili akamsaidia kumkalisha kwenye kiti huku akimpa pole nyingi au tuseme za kumwaga. Si mpenzi wake, sasa je?
“Mama Pilima,” aliita baba Pili kwa sauti ya kumdekeza aliyemwita.
Mama Pilima alikuwa amejiinamia tu kwenye meza. Muda huo, uso wake ulikuwa bado una aibu maana alitambua kwa nini alianguka na kuzimia. Mkoba wake na viatu vyake viliwekwa katika hali ya usalama…
“Mama Pilima,” aliita tena baba Pili, safari hii kwa sauti ya kubembeleza…
“Abee…”
“Pole sana…”
“Asante.”
“Pole sana,” safari hii alisema baba Pilima.
“Asante,” mama Pilima, bila aibu wala soni, achilia mbali haya, eti aliitikia pole ya mumewe…mh!
“Kwani ulijisikiaje?” aliuliza baba Pili.
Kabla mama Pilima hajajieleza, baba Pilima akadakia…
“Bwana Mutu…”
“Naam bwana Emmanuel…”
“Mimi nadhani acha niende, shemeji akiwa ametengemaa, nipigie simu nikuletee mzigo mahali popote pale utakapokuwa…”
“Bwana Emmanuel naweza kukuruhusu, nitakujulisha kila kitu,” alisema baba Pili huku baba Pilima akisimama na kuondoka zake…
“Pole sana,” alimpa pole nyingine mke wake na kuanza kutembea.
Nyuma sasa, baada ya kupita kama dakika tano nzima bila kuwepo wa kuongea, ukimya ulikatika…
“Mama Pilima…”
“Abee…”
“Ni nini kwani mpenzi wangu?”
Mama Pilima kabla hajajibu, aligeuka kuangalia geti kuu, nadhani kujiridhisha kama mumewe alishaondoka kabisa eneo lile…
“Baba Pili, unamjua yule?”
“Eee…anaitwa Emmanuel.”
Mama Pilima alitingisha kichwa cha kukataa kwamba, yule si Emmanuel…
“Yule anaitwa Marco…”
“Marco? We unamjua? Au umemfananisha?”
“Namjua…”
“Ni nani?”
Kabla mama Pilima hajafunguka simu ya baba Pili iliita, aliyepiga ni baba Pilima kwani aliseviwa kwa jina la Emmanuel…
“Subiri kwanza nimsikie huyu mgeni aliyeoondoka,” aliomba baba Pili…
“Haloo bwana Emmanuel…”
“Mimi si Emmanuel, naitwa Marco au baba Pilima…”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baba Pili alikata simu ghafla, akamtumbulia macho mama Pilima…
“Ina maana huyu jamaa ni mumeo?” alimuuliza mama Pilima…
“Ndiyo,” mama Pilima alijibu kwa mkato.
“Mh! Usitake kuniambia mama Pilima. Ina maana amejua kila kitu?” aliuliza tena baba Pili…
“Siyo amejua kila kitu, bali nahisi amepanga kufanya hivi…we unafahamiana naye?” mama Pilima alimuuliza baba Pili…
“Simfahamu…yaani ilikuwa hivi…”
Baba Pili alianza kumsimulia kila kitu mama Pilima huku akionekana kuwa na wasiwasi sana. Mama Pilima naye alikuwa na wasiwasi mkubwa. Kwanza alijua mume wake hakwenda mbali na angerudi kwa njia ya fumanizi sasa.
Hivyo alikuwa na mchecheto…
“Sasa mimi naona niondoke zangu,” alisema mama Pilima huku akisimama. Ni baada ya maelezo ya baba Pili ambapo ilibainika wawili hao siyo watu wanaojuana, hivyo mama Pilima akajua kuna kitu.***
Baba Pilima alipotoka hapo alimpigia simu baba Pilima feki…
“Mambo ndugu yangu?”
“Poapoa, nani mwenzangu?”
“Mimi naitwa Juma Ally. Namba yako nimepewa na rafiki yako, anaitwa Juma kama mimi…uko wapi nikuone? Nina biashara nataka kufanya na wewe!”
Alipoulizwa hivyo, awali alijiuliza Juma Ally alikuwa nani na alitaka kufanya naye biashara gani, hakupata jibu.
Kwa kuwa alipozi sekunde kadhaa bila kuendelea kuzungumza na aliyempigia simu, baba Pilima akamwambia;
“Vipi ndugu yangu mbona huzungumzi, muhimu sana tuonane leo kwani kesho natarajia kusafiri.”
Baba Pilima feki alipoambiwa hivyo akaona kabla ya kuendelea na mazungumzo amwulize ni Juma yupi aliyempatia namba yake;
“Oke…namba yangu amekupa Juma yupi? Maana kuna Juma wa Kimara na Juma wa Mbezi Beach!”
“Mh! Yule sijajua anaishi Mbezi ipi!”
“Anyway, wewe njoo mpaka Buguruni, kuna baa inaitwa Sewa, mimi nipo hapa.”
“Hapo Sewa unatarajia kukaa kwa muda gani maana nipo mbali kidogo?” baba Pilima feki alimwuliza.
“Mimi nitakusubiri muda wowote, kikubwa nataka kuonana na wewe leo,” baba Pilima alimwambia.
“Sawa.”
Baba Pilima aliharakisha kufika Buguruni mpaka kwenye baa hiyo, akazama ndani na kumkuta baba Pilima mwenzake amekaa na washkaji wake watatu, akiwemo Juma mmoja.
Baada ya salamu, baba Pilima feki akasema…
“Sasa wewe namba yangu utakuwa umepewa na Juma wa Mbezi Beach, maana Juma wa Kimara ni huyu hapa…”
“Oke…oke…oke! Sawa.”
“Sasa jamani ngoja nikae na mgeni wangu pembeni kidogo,” alisema baba Pilima huku akisimama, akaenda kukaa meza nyingine na baba Pilima mwenyewe…
“Enhee, niambie ndugu yangu…ulisema unaitwa..?”
“Juma Ally.”
“Haya Juma Ally niambie.”
***
Mama Pilima kule Kariakoo hakupenda kurudi nyumbani bila kukutana na mumewe kwanza na kuzungumza naye ili ikibidi mambo yaishe ndipo aweze kufika nyumbani…
“Yaani bila kumaliza haya mambo sidhani kama nitaweza kurudi nyumbani. Hali yangu itakuwa mbaya mimi,” alisema moyoni mama Pilima. Alimpigia simu…
“Sorry… ngoja nipokee simu ya mke wangu kwanza,” alisema baba Pilima…
“Oke…oke…”
Baba Pilima alimpokelea mkewe…
Lakini wakati huohuo, simu ya baba Pilima feki iliita, aliyepiga ni baba Pili, pacha wake. Alitaka kumpasha kilichomtokea lakini baba Pilima feki hakupokea kwa sababu baba Pilima au Juma Ally alikuwa akiongea na mkewe, akamtumia meseji…
“Nitakupigia niko na mgeni wangu mara moja.”
“Poa,” alijibu baba Pili…
“Uko wapi baba Pilima?” mama Pilima alimuuliza mke wake…
“Niko Buguruni…”
“Naomba nije tuonane please…”
“Njoo.”
“Oke, Buguruni sehemu gani?”
“Kuna baa inaitwa Sewa.”
“Poa.”
Baba Pilima mwenyewe alimshukuru Mungu wake akijua amemaliza kazi maana mkewe amejiingiza mwenyewe kwenye mtego wake…
“Enhe, niambie bwana Juma,” alisema baba Pilima feki huku akikaa sawasawa au akikaa vizuri.
“Mimi ninashughulika na biashara ya mbao, sasa niliambiwa wewe unajua wateja wanaolipa sawasawa…sijui ni kweli?” alianza kusema baba Pilima mwenyewe.
Baba Pilima feki alimtumbulia macho pima, maana yeye si mfanyabiashara kabisa, sasa hata kama ni kweli alipewa namba na Juma wa Mbezi Beach, mbona naye anajua yeye si mfanyabiashara!!
“Da! Umenipeleka mbali sana bwana Juma Ally…kwanza kama kweli Juma ndiyo amekupa namba yangu mbona anajua mimi siyo mfanyabiashara au alikosea akakupa namba yangu?”
“Mimi sijui,” alijibu baba Pilima mwenyewe. Alishaanza kuwa na wasiwasi sasa.
Akashika simu yake na kuandika namba za rafiki yake Juma wa Mbezi Beach ili amuulize kisa cha kutoa namba yake kwamba anawajua wateja wa mbao wakati anajua yeye si mfanyabiashara.
Baba Pilima mwenyewe alitaka kumzuia, lakini moyoni akasema aache tu, atapambana mpaka mwisho na vile mkewe yuko njiani, mshindi atakuwa yeye tu…
“Haloo Juma…” alianza kwa kuita baba Pilima feki…
“Haloo, niambie…”
“Eti unamfahamu jamaa anaitwa…”
Kabla hajamaliza kusema, simu yake ilikatika kwa sababu ya mtandao, akapiga tena.
Simu iliita sana, lakini haikupokelewa upande wa pili.
Simu ya baba Pilima mwenyewe ikaita, mkewe alishafika…
“Nipo hapa nje ya Baa ya Sewa…”
“Ingia ndani sasa.”
“Poa.”
Mama Pilima alizama ndani na kushtuka kumwona baba Pilima mumewe akiwa amekaa na baba Pilima feki…http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ha!” alihamaki mama Pilima, akaanguka tena.
Baba Pilima feki alishtuka sana. Alishtuka kwa mambo mawili. Kwanza kwa kumwona mama Pilima, pili kwa kuanguka…
“He! Huyu mwanamke namfahamu, ni mwanamke wangu, sasa sijui imekuwaje tena na sijui amekuja kufuata nini hapa?” alihoji baba Pilima feki huku akimtumbulia macho mama Pilima pale chini…
“Wewe ni mwanamke wako, mimi ni mke wangu,” alisema baba Pilima mwenyewe. Baba Pilima feki naye akaanza kuweweseka huku jasho jembamba likimtoka…
“Ina…ina…ina maana…ina maana,” alisema baba Pilima feki ambaye kwenye simu ya mama Pilima aliseviwa kwa jina la Baba P…
“Usisumbuke sana ndugu, kaja hapa kwa sababu yangu na mimi nimekutafuta wewe kwa sababu ya yeye. Wewe ndiye Baba P, unatembea na mke wangu huku ukijua ana mume…muda si mrefu nimetoka kwa Baba Pili…nadhani ni mapacha maana hata sura zenu zinafanana,” alisema baba Pilima huku akiwa amekasirika sana.
Watu walimzunguka mama Pilima, baba Pilima mwenyewe akiwa anamsaidia mkewe akae kwenye kiti maana safari hii hakupoteza fahamu kama kule DDC-Kariakoo…
“Pole sana jamani…pole,” watu walimpa pole mama Pilima akiwa amekaa kwenye kiti…
“Baba Pilima mume wangu,” aliita mama Pilima kwa sauti ya chini sana ikiashiria kuchoka na mambo yalivyokwenda…
“Nini?” baba Pilima alimjibu hivyo mke wake…
“Nimekukubali mume wangu. Hata kama leo utanipa talaka lakini nitakuheshimu kuliko mwanaume yeyote hapa duniani. Najua kukutana wewe na yule mwanaume Kariakoo ilikuwa mbinu yako, lakini pia kukutana na huyu hapa pia ni mbinu yako japokuwa mimi nimejikuta nikiingia kichwakichwa…
“Sikutaka kukusaliti. Imetokea tu! Lakini si kwamba sikupendi na huenda labda ni kwa sababu ya mambo yetu ya siri nyumbani…nisamehe kwa utangulizi lakini uamuzi ni wako ingawa mimi kama mimi ningependa unisamehe,” alisema mama Pilima huku akiona aibu kwa watu waliokuwa wakimsikiliza.
Baba Pilima alimwangalia mkewe kwa macho ya kumshangaa sana kisha akasema…
“Umemaliza kusema?”
“Nimemaliza baba Pilima mume wangu.”
“Kwa hiyo kama kuna matatizo nyumbani ndiyo ukaamua kutembea na mapacha?”
“Hiyo nayo ni stori ndefu mume wangu, inataka nafasi ya kusimulia kwa mapana,” alisema mama Pilima huku akizidi kuona aibu.
Baba Pilima alisimama, akamuaga baba P kwamba anaondoka huku akisema…
“Mkubwa mimi sifanyi biashara yoyote. Sina mbao wala miti. Ila nilitaka kukuona. Nimejikaza sana katika hii ishu.
Ningekuwa mwanaume mwingine nadhani ningeua mtu au ningeua watu. Lakini mjue kwamba mimi ni binadamu kama binadamu wengine, sijapenda mlichonifanyia. Nasema sijapenda kwa sababu wote mlijua huyu ni mke wa mtu japokuwa hata yeye alitakiwa kujijua kwamba ni mke wa mtu. Naye ana nafasi yake ya lawama.”
Wakati baba Pilima akimalizikia kutoka nje ya baa hiyo, mama Pilima kule ndani aliangua kilio huku naye akisimama…
“Nilishasema mimi sijawahi kusaliti jamani. Sijui shetani gani amenikuta katika kipindi hiki cha kuelekea uzeeni. Kwani kama ningemvumilia mume wangu na udhaifu wake nini kingenipata mama Pilima!”
Watu waliojua kisa hicho walimzomea mama Pilima huku baba P akibaki kushangaa. Simu yake ikaita, alipiga baba Pili…
“Haloo,” alipokea baba P…
“Ndugu yangu yamenikuta mazito,” alisema baba Pili…
“Nadhani hayo yako ni madogo, mimi zaidi…mwenzako si nimefumaniwa na mume wa mama Pilima…” alisema baba P.
yaani we acha tu…haya wewe mwenzangu yamekupata makubwa yapi?” alisema baba P…
“He! Mume wa mama Pilima?”
“Ndiyo…”
“Mbona hata mimi pia imekuwa hivyo…”
“Wewe lini?”
“Muda si mrefu ndugu yangu.”
Simu ya mama Pilima iliita akiwa nje ya baa hiyo, alipoangalia mpigaji ni mume wake…
Aliipokea huku akitetemeka…
“Halo baba Pilima…”
“Najua umeona ushatani wako ulipokuwa. Umekuwa mwaminifu miaka yote unakuja kuanguka mbeleni huku mke wangu…”
“Nisamehe baba Pilima…”
“Kwanza ujasiri wa kutembea na wanaume wawili umeutolea wapi mke wangu?”
“Baba Pilima ni hadithi ndefu, wale akina kaka ni mapacha. Walitumia nafasi hiyo kunipata wote nikiwa sijui kama ni mapacha,” alisema mama Pilima akitumia sauti ya chini sana yenye kuonesha majuto ni mjukuu…http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sikiliza mama Pilima, mimi kutoka moyoni mwangu nimekusamehe!”
Mama Pilima alianguka chini nje ya kituo cha mabasi, watu wakaanza kutafutana. Habari za kuanguka kwake zilifika hadi ndani ya Baa ya Sewa ambapo, baba Pilima feki ni mmoja wa watu waliosikia, lakini hakujua ni nani!
Alipotoka kuangalia na kumkuta ni mama Pilima alishtuka sana. Lakini kwa sababu ya mambo yaliyotokea hakutaka kumsaidia wala kuendelea kusimama kuendelea kuangalia pale…
“Mh! Huu ni msala. Jamaa yake akitokea inaweza kuwa balaa,” alisema moyoni baba Pilima feki huku akiondoka zake eneo hilo.
Baba Pilima alishangaa sana mkewe kukatika hewani ghafla halafu huku akisikia kishindo kikubwa cha puu! Alipojaribu kumpigia hakuwa hewani…
“Khaa! Sasa huyu amekumbwa na kitu gani tena?” alijiuliza baba Pilima.
Baadhi ya vijana wa kihuni waliinyakua simu ya mama Pilima na kutokomea nayo wakiwa wameshaizima na ndiyo maana mume wake hakumpata tena hewani.
Kutokana na tukio hilo la aina yake, baba Pilima mwenyewe aliamua kurudi nyumbani kupumzisha akili siku hiyo huku akimuwaza mkewe na alichokifanya. Lakini bado ndani ya moyo wake aliamini, yaliyotokea yamekuwa funzo kwa mwanamke huyo.
***
Ndani ya dakika kumi, mama Pilima naye aliamka. Au alizinduka. Ama fahamu zilimrejea, akakaa na kuangalia kulia na kushoto, mbele na nyuma na kubaini nini kilimtokea muda mfupi nyuma.
Mkoba wake ulikuwepo, lakini simu hakuiona. Miongoni mwa watu waliokuwa wakimfuatilia pale chini ni wanawake wenzake na watu wazima tu, vijana wote, wakiwemo wa kihuni walikuwa hawana habari…
“Simu yangu,” alisema mama Pilima…
“Watakuwa wameikwapua vibaka,” walisema watu.
Mama Pilima alisimama kwa kujizoazoa, akapanda basi na kukaa siti ya nyuma kabisa akiwa peke yake. Baadhi ya sehemu za nguo zake zilichafuka kutokana na kuanguka…
“Kweli baba Pilima anaweza kunisamehe kwa kosa kubwa kama hili? Hata siamini! Labda nilimsikia vibaya,” alisema mwanamke huyo akiwa kweli haamini kama amesamehewa.
Alipofika nyumbani, alimkuta mumewe, baba Pilima, wifi yake pia alikuwepo sebuleni. Msichana wa kazi akiendelea na kazi za kupika. Watoto, akiwemo Pilima walikuwa hawajarudi toka walikokwenda.
Wifi mtu alishtuka sana kumwona mama Pilima amechafuka vile…
“Ha! Wifi…umekutwa na jambo gani? Mbona umechafuka?”
Mama Pilima alimwangalia mumewe badala ya aliyemuuliza swali. Alijua mumewe atasema yote…
“Wifi nilianguka nikapoteza fahamu,” alisema mama Pilima na kuanza kulia.
Ikawa hekaheka nyingine, wifi mtu huyo akiwa anataka kujua kwa undani kuhusu wifi yake kuanguka ghafla na kupoteza fahamu…
“Haa! Kaka! Wewe unajua lolote?”
“Nilikuwa naongea naye, lakini ghafla akapotea hewani. Nilipokuwa nampigia tena, hakuwa hewani. Nadhani ndiyo alianguka hapo.”
“Wifi…”
“Abee…”
“Pole sana. Sasa simu iko wapi?”
“Imeibiwa wifi,” alisema mama Pilima.
Baba Pilima alimshika mkono mke wake mpaka chumbani. Alimvua nguo, akamvalisha kanga na taulo na kumtaka akaoge.
Baada ya kuoga, mama Pilima na mumewe wakakaa chumbani…
“Mume wangu, asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Kwa haya yaliyonikuta mimi nimefunzwa tayari. Nataka kusikia kauli yako kwa mara ya pili kama kweli umenisamehe.”
“Nimekusamehe mama Pilima. Ila likijirudia jambo hilo tena, itakuwa tiketi yetu ya kutengana moja kwa moja,” alisema baba Pilima.
Mama Pilima alipiga magoti, akaweka mikono pamoja kaka anayesali, akamsihi mumewe kuwa na amani. Ujinga ule hautajirudia tena.
“Naomba iwe hivyo katika maisha yako yote.”
“Nakuahidi itakuwa hivyo baba Pilima.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa upande wa wale mapacha, baba Pilima feki na baba Pili walikwenda kukutana sehemu. Wakaongelea lile tukio, wakakubaliana kuzitupa laini zao na kununua mpya ili wasitafutwe. Walijuta na kujuta na kujuta!
MWISHO.
0 Comments